BADGE

Tuesday, June 1, 2010

Israel kuchunguzwa na Umoja wa Mataifa

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetaka kuanzishwa uchunguzi huru kufuatia shambulio kwenye meli za kibinadamu zilizokuwa njiani kupeleka misaada katika ukanda wa Gaza.
                                                   Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Taarifa ya Baraza la Umoja wa Mataifa imetokea baada ya mashauriano yaliyochukua usiku kucha. Takriban wanaharakati 10 waliuawa wakati wanajeshi wa Israel walipoingia ndani ya meli hizo kwenye mipaka ya kimataifa.
Taarifa hiyo imeafikiwa kati ya Uturuki na Marekani, huku Uturuki ikisisitiza laana kali dhidi ya Israel nayo Marekani ikaamua kutotoa maneno makali kwa mshirika wake huyo wa karibu.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani matukio yote yaliyosababisha vifo vya watu 10 na wengine wengi kujeruhiwa pamoja na kufariji familia za waathirika.
Aidha baraza hilo limetaka meli hizo ambazo zinazuiliwa mwambao wa Israel kuachiliwa mara moja. Punde baada ya taarifa hizo kutolewa wapiganaji kadhaa wa Kipalestina walivuka mpaka na kuingia upande wa Israel ambapo walikabiliana na wanajeshi huku wawili wakiuawa.
Kwa upande wake mwakilishi wa Israel katika Umoja wa Mataifa amesema wanajeshi wake walikuwa wakijikinga kutoka mashambulio ya wanaharakati hao.